Wakati kukiwa na malalamiko ya wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi kudaiwa kuhusika katika mauaji ya watuhumiwa wanaokamatwa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imeingilia kati suala hilo na kupendekeza makosa yote ya jinai yanayowahusu askari polisi yachunguzwe na taasisi nyingine huru za umma.
Tume hiyo imelitaka pia Jeshi la Polisi lihakikishe utendaji wake wa kazi unazingatia sheria, kanuni na miongozo ya utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.
Walipotafutwa kuzungumzia mapendekezo hayo ya tume, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na msemaji wa jeshi hilo, David Misime hawakupatikana mara moja, licha ya jitihada za kuwapigia simu na kuwatumia ujumbe mfupi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni alisema aliunda timu maalumu kuchunguza malalamiko aliyoyapokea ya mauaji yanayofanywa na polisi na tayari imemkabidhi ripoti kwa ajili ya utekelezaji.
“Nataka nikupe tu taarifa kwamba mimi nilishaunda hiyo timu na imefanya hiyo kazi ya kuchunguza malalamiko ambayo niliyapata kama waziri au niliyosikia kupitia vyombo vya habari na ile timu ilihusisha watu kutoka taasisi mbalimbali, na tayari imeniletea ripoti yake na nimeshaanza kuifanyia kazi,” alisema Masauni.
Waziri huyo aliongeza kwamba Jumatatu ijayo, atakutana na uongozi wa Jeshi la Polisi nchini ukiongozwa na IGP Sirro na timu yake ili kujadiliana haya matukio ambayo yamejitokeza hivi karibuni ambayo hayakuwepo kwenye ripoti ya tume yake.