Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wanne imeahirishwa hadi Julai 4, 2022 kutokana na upelelezi kutokamilika.
Sabaya na wenzake wanne walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi leo Juni 20,2022 kwa ajili ya kesi yao kutajwa.
Akiomba kuahirishwa kwa kesi hiyo wakili upande wa mashtaka, Verediana Mlenza ameieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba kibali kutoka ofisi ya DPP na hati ya kuipa mahakama hiyo mamlaka ya kuendelea na kesi hiyo bado hakijatolewa.
Kabla ya kuombwa kwa ahirisho hilo wakili wa upande wa utetezi, Hellen Mahuna aliutaka upande wa mashtaka kuwa makini kwa sababu mara ya kwanza washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka yao walieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi umeshakamilika.
“Hatuna pingazmizi na ahirisho, upande wa mashitaka mara ya kwanza kesi ilipoletwa katika mahakama hii walieleza kuwa upelelezi umeshakamlika ,mara ya pili wakaja hapa na kutuambia upelelezi bado haujakamilika sasa ni mwezi, tunaomba upande wa jamhuri wawe “serious”,kwa sababu washtakiwa wanateseka,” amesema.