Wazee Bunda wajiundia Chombo cha kutetea maslahi yao

Sylvia Ndamugoba na Jessica Mwita

Wananchi wa Mtaa wa Bunda Stoo uliopo mjini Bunda,katika mkoa wa Mara, wameunda Baraza litakaloratibu misaada kwa wazee. Baraza hilo pia litawawezesha wazee hao kufahamu na kutambua haki zao, zikiwemo zile za kupata huduma za Afya.

Akizungumza Ijumaa juma lililopita katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Mji wa Bunda, Afisa Mtendaji wa Kata ya Bunda Stoo, Raymond Bukombe, amesema lengo la kuunda Baraza hilo ni kusikiliza kero zinazowapa wazee katika jamii.

“Wazee wengi wamekuwa wakikutana na changamaoto hasa wanapougua na kufika katika Zahanati na Vituo vya Afya kutafuta tiba, na hakuna chombo mahsusi cha kuwasaidia”,amesisitiza Afisa Mtendaji huyo.

Baadhi ya wawakilishi wa wazee wamesema kuwa kuudwa kwa baraza hilo kutawasaidia wazee wenye umri kuanzia miaka sitini na kuendelea waweze kupata huduma sahihi hususani vijijini.

Hata ivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee hao, Zacharia Katondo, ameishukuru serikali kwa kuwatambua wazee katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, kuona kuwa wanaweza kuwa na mchango wa kuisaidia serikali na jamii.

Author: bundafm