MIAKA MINNE YA JPM


                        MIAKA MINNE YA JPM

               Na Conges Mramba,Bunda FM Radio

NOVEMBA 5 mwaka huu 2019,Rais Dk.John Pombe Magufuli ametimiza  miaka minne kamili tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Magufuli aliapishwa Novemba 5,mwaka 2015.

Ingawa kuna kelele nyingi za mabeberu kwamba utawala huu unakandamiza Haki za Binadamu, sisi wengine tunautazama kwa mtazamo chanya.

Katika Miaka mitatu tu  ya Rais Magufuli, serikali ilikuwa imeondoa msongamano wa magari katika Barabara  za miji mikubwa hapa nchini Tanzania, Mwanza barabara inayokwenda uwanja wa ndege ilikuwa imepanuliwa.

Barabara hii ilikuwa finyu(njia mbili),magari yalikuwa yakishindwa kutembea, hasa nyakati za asubuhi na jioni, watu walipokwenda au kurejea nyumbani  kutoka makazini.

Katika eneo la Ghana,kulikuwa na ajali nyingi zikitokea,kufuatia watembea kwa miguu kuvuka barabara katika eneo hilo.

Ni kama ilivyokuwa katika eneo la Natta,kabla ya ‘Fly Over’ kujengwa,kulikuwa na ajali nyingi.

Katika siku za mwanzo za Utawala wake, Rais Magufuli alifika Mwanza na kusema:

“Zile fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano, sasa zingepanua Barabara hii na kujenga Daraja la waenda kwa miguu, ili kuokoa maisha ya wananchi yaliyokuwa yakiangamia kila siku”.

Mradi wa Ujenzi wa Barabara Ghana,Mwanza

Wakosoaji waliinuka kusema, “Rais alikuwa akitumia mabavu,kuchukua fedha(takriban shilingi bilioni mbili)zilizokuwa hazijaidhinishwa na Bunge,kwenda kujenga Barabara Mwanza”.

Rais aliwajibu wakosoaji wake kwamba, fedha zile zilikwishapangiwa matumizi na Bunge,(Sherehe), na kwamba Barabara ile inapopanuliwa hata wao wangeepuka msongamano wa magari,na wangekuwa wanawahi safari za ndege-Barabara hii ndiyo inayokwenda uwanja wa ndege wa Mwanza,ambao nao umepanuliwa, Ujenzi  wa uwanja huu umekamilika.

Leo, serikali ya Rais Magufuli ina mpango wa kujenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa katika eneo la Igegu huko Bariadi Mkoani Simiyu.

Mkataba wa ujenzi  wa Barabara hizi(Makongoro kwenda Uwanja wa Ndege,kuanzia Mwaloni)ulisainiwa Aprili 18, mwaka 2017; Kampuni ya Nyanza Road Works ikapewa kandarasi kwa gharama ya shilingi 9,542,701,531.96.

Hadi sasa ujenzi umefika asilimia zaidi ya 70,na kama siyo TANESCO kuchelewesha mradi huo kwa kukataa kuondoa nguzo barabarani, ulikamilika  na ulipangwa  kukabidhiwa Mei mwaka jana  2018.

 Leo,  miaka minne baadaye sakata hilo la Magufuli kuchukua bilioni mbili za Sherehe za Muungano na kujenga Daraja la Waenda kwa miguu(Fly Over) Ghana,jijini Mwanza siyo tena ajenda.

Eneo  hili la Ghana ni mahali wapiga picha wanapojipatia kipato chao kwa kupiga picha.

Vijana wengi hushinda mahali hapa wakipiga picha, ‘Tik Tik Tik’ wanalipwa na watalii  mbalimbali wanaofika hapa kushangaa!

Rais Magufuli wakati wa Uzinduzi wa daraja hili la waenda kwa miguu aliwatania ‘ndugu zake’ Wasukuma,

“Ndugu zangu Wasukuma, daraja hili sasa patakuwa mahali pa ninyi kufungia ndoa hapa!”

Watu(Kicheko cha kuvunja mbavu)

Mradi huo unafurahiwa na kila Mtu hivi leo,‘Udikteta wa Magufuli’ umeondoa adha ya msongamano wa magari Mwanza, ‘Fly over’ hiyo ilishazinduliwa,licha ya kuokoa maisha ya wananchi, ni kivutio kikubwa na chanzo cha ajira kwa wapiga picha zaidi ya 100.

Mradi huu wa upanuzi wa Barabara ya Uwanja wa ndege,ulikuwa uende sambamba na ujenzi wa Barabara ya Kabuhoro-Ziwani, ni eneo hili la Kirumba.

Mradi huu ni moja tu ya miradi mikubwa kama reli ya kisasa(SGR) na mradi wa umeme wa Rufiji,nasikia unaitwa Mwalimu Nyerere.

Mwanza kuna ujenzi wa madaraja makubwa, kama lile la Busisi-Kigongo Ferry, kuna Ujenzi wa Bandari ya Nchi Kavu,Fela wilayani Misungwi,kuna ujenzi wa daraja la Mto Simiyu(Magu),Upanuzi wa uwanja wa ndege n.k

Daraja la chuma la Mto Simiyu linapanuliwa ili magari yaweze kupishana darajani.

Mhandisi M/S Core Consulting Engineering ya Ethiopia na Luptan ya Tanzania,watajenga upya daraja hili kwa gharama ya shilingi 375,650,000.

Barabara ya Musoma kuanzia Nyanguge(Magu) inakarabatiwa.

Barabara hii ilijengwa mwaka 1986,sasa inabanduliwa lami na kuwekewa lami mpya kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5.

Meli mpya inajengwa,nyingine mbili zinakarabatiwa, ili kuhakikisha Reli Mpya ya kisasa(SGR)itakapofika Mwanza,basi usafiri wa meli uwe umejipanga kusafirisha bidhaa na abiria kuanzia Mwanza kwenda kote nchi za Maziwa Makuu.

Sitazungumza ununuzi wa ndege nane za serikali ambazo wanakabidhiwa Shirika la Ndege(ATCL).

Nitajadili  kuhusu meli katika maziwa makuu ya Victoria na Tanganyika.

Hata ziwa Tanganyika meli kongwe Mv.Liemba iliyojengwa Ujerumani miaka ya mwisho ya 1800 ikasafirishwa kwa meli hadi Dar kisha kwa treni hadi Kigoma, ikazamishwa vilindini ziwa Tanganyika kwa miaka mitatu, sasa inakarabatiwa vizuri.

Bandari ya Nchi Kavu inajengwa Fela wilayani Misungwi.

Bandari hii,meli mpya na zinazokarabatiwa na Reli ya SGR vikikamilika, ni mkakati wa kiuchumi wa kufungua lango la biashara ya Kimataifa na nchi zote za Maziwa Makuu.

 Kampuni ya Meli(MSCL)ilikuwa ikihujumiwa na ‘wajanja’ ikafilisika,wakati ‘akina Mafuru’ wanaoendesha usafiri hapa ziwani kwa kutumia mitumbwi,wakijiendesha kwa faida!

Utawala wa Magufuli wa miaka mine umeleta yafuatayo:

Kampuni hii sasa imepewa Menejimenti mpya.

Afisa Mtendaji Mkuu(CEO)Eric Hamissi,ameapa kuhakikisha meli zake zinakuwa kiungo kikubwa cha uchumi hapa nchi za Maziwa Makuu.

Miradi hii ya kimkakati inahujumiwa wakati wakuu wa wilaya na mikoa wapo, wanatazama tu.

Ingawa Rais anakwenda Mwendo wa haraka, nakiri bado wapo watu ambao wanakwenda mwendo wa pole,wakiambiwa “Heshimaaz- toa”,wao wanageuka kushoto!

Nadhani hawa ni ‘mananga’ wanaostahili kupumzishwa, ‘gwaride’ limewashinda! Hawawezi kuendana na Kasi hii ya Rais Magufuli.

Upanuzi wa uwanja wa ndege Mwanza, unaofanywa na Kampuni ya Kichina, BCEG chini ya Mhandisi Mshauri, Unitec Limited ya Dubai,umechukua muda mrefu,ingawa inasemwa mradi huu umefika asilimia takriban 100.

Hiki ni kiwanja muhimu cha tatu nchini, kati ya viwanja 58 vilivyo chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege(TAA).

Ni cha tatu nyuma ya Julius Nyerere International Airport(Dar es salaam) na Kilimanjaro(KIA).

Abiria 203,045 wanawasili hapa kila mwaka, wengine 219,303 wanasafiri kupitia hapa;wakati wastani wa tani 2,170 za mizigo husafirishwa kwa ndege kutoka hapa.Hizi ni pamoja na samaki na madini-utajiri wa Mwanza.

Huu ndiyo uwanja wa ndege wa kwanza ndege ya Air Tanzania “Tango Cherie,” yenye jina ubavuni,Kilimanjaro, ilipotekwa hapa miaka ya 80 na ‘Waziba matairi wa Mwanza’ na kupelekwa London!.

Hapa sasa, serikali inaimarisha miundombinu muhimu ya kiusalama,ili watu wote wanaotaka kwenda Ulaya wasipite Dar es salaam,waondokee hapa.

Mradi huu umechukua miaka mingi, tunahisi kuna ‘Wapigaji’.

Dk. Magufuli,mwaka 2013 alipofanya ziara hapa akiwa Waziri wa Ujenzi,alitishia kumtimua Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kwa kuchelewesha ujenzi.

Rais aliagiza barabara inayoanzia hapo kwenda Kayenze ijengwe kwa kiwango cha lami, lakini anapoondoka tu, nyuma hakuna kinachoendelea!

Bado wanacheza, ‘Makida makida’.

Kuna baadhi ya watendaji serikalini bado hawaimbi wimbo mmoja na Rais,ili kuwaletea maendeleo wananchi wa  Tanzania kwa kasi ile ya ‘Tanzania ya Magufuli’,yenye kasi  kuendea maendeleo.

MAGUFULI AMEJENGA DARAJA LILILOVUNJIKA

Serikali ya Awamu ya Tano, inayotaka Tanzania kuchupa kwenda Uchumi wa Viwanda, sasa  imefungua milango ya kuingia  Nchi zote za Maziwa Makuu.

Kenya,Uganda,Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Burundi na Zambia na Malawi, zitaunganishwa na Tanzania kupitia Reli ya Kati na Meli za Maziwa Makuu,zitafikiwa  kirahisi.

Kwa takriban miaka 10, Tanzania ilikuwa imejifungia milango ,baada ya Reli ya Kati na Meli 14 zilizomo katika maziwa yake yote makubwa(Victoria,Tanganyika na Nyasa),kuacha kusafirisha abiria na mizigo kwenda na kutoka  nchi hizi.

Matokeo yake, uchumi ulishuka hata mfumuko wa bei ukawa mkubwa.

Azma ya Rais,Dkt.John Magufuli,kufufua Reli ya Kati, na Kujenga Mpya ya kisasa, Standard Gauge, kisha Kujenga Meli Mpya mbili na kufufua  nyingine tano katika maziwaNyasa, Tanganyika na Victoria, sasa ni ishara ya cheche za uhai wa uchumi kurejea kutembea, mithili ya mishipa ya damu katika mwili.

Ukanda wa Ziwa ni  kitovu(hub) cha Uchumi na Usafiri katika nchi zote za Maziwa Makuu:

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Rwanda,Burundi,Kenya,Uganda, na Nchi za SADC zikiwemo Zambia na Malawi.

Eneo hili nn Kitovu(hub)cha Uchumi hapa Maziwa Makuu, na kwakuwa ni kituo cha viwanda vya Bidhaa za Nje, Export Processing Zone(EPZA),Reli ya Kati inayofufuliwa, na Reli Mpya ya Standard Gauge inayojengwa,ikifika hapa Uchumi wa watu wa kawaida utakua maradufu.

Bandari ya Nchi Kavu inayojengwa Fela wilayani Misungwi,Usafirishaji wa abiria na Mizigo kutoka relini kuingia Meli zilizomo ziwa Victoria ni kichocheo cha Uchumi kwa wakazi wote wa eneo hili.

 “Hata wenye nyumba za kulala wageni na mama ntilie,watapata faida katika biashara yao, hata wanaofanya biashara ndogo ndogo watanufaika”,Kiongozi mmoja wa serikali mkoani Mwanza aliwahi kusema.

Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni ya Meli nchini,MSCL,Philemon Bagambilana, alisema, Usafirishaji wa bidhaa kutoka Pwani kwenda Nchi hizi za Maziwa Makuu,kupitia Ushoroba wa Kati(Central Corridor) ni salama zaidi kuliko nchi nyingine yoyote, kufuatia Tanzania kuwa na amani wakati wote.

“Kwa kuwa Tanzania ni nchi tulivu, hata usalama wa mizigo kwenda nchi hizi ni mkubwa kuliko nchi jirani”, Bagambilana anasema.

Kauli hii, inafuatia ukweli kwamba,mizigo ya Rwanda na Uganda iliyokuwa ikipitia Bandari ya Bombasa, imekuwa ikikumbana na hasara kutokana na ukosefu wa Usalama mpakani mwa Kenya na Uganda,hususan Magharibi mwa Kenya ambako kumekuwa kukitokea mapigano ya kikabila.

Aidha, Kampuni hii ya Meli nchini,MSCL inasema, shehena inayopita kutoka reli ya kati,kisha kusafirishwa kwa meli hadi Kampala,huchukua siku zisizozidi tatu.

“Tumekubaliana kuwa na tozo moja,na kutoka Bandarini hadi Kampala,mzigo ufike katika muda wa siku tatu tu”,anafafanua Meneja Biashara na Masoko wa MSCL yenye Makao yake jijini Mwanza.

Imesemwa pia kwamba,Usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam hadi nchi za Maziwa Makuu kwa kutumia reli na meli,kutapunguza uharibifu mikubwa wa barabara za lami zilizokuwa zikiigharimu nchi  matengenezo ya mabilioni ya shilingi kila mara.

Tayari Meli ya Mv Umoja,imeanza kusafirisha shehena ya mizigo kwenda Port Bell, ambako pia husafirishwa na reli kwenda Kampala mji Mkuu wa Uganda.

Mara ya mwisho,Meli hii ilisafirisha shehena ya mizigo kwenda Port Bell na Jinja, Uganda,Agosti 21 mwaka 2009. Kuanzia mwaka 2009, hadi mwaka jana tu(2018) Tanzania haikuwa na usafiri wa meli wala reli za mizigo kwenda Uganda.

Unaposema usafiri huu unazungumzia pia uwezekano wa kufika Juba(Sudan Kusini),Congo,Burundi na Rwanda.

Kwa takriban miaka 10,usafirishaji wa mizigo kati ya Mwanza na Kisumu nchini Kenya au Jinja na Port Bell nchini Uganda,ulikuwa umesitishwa kufuatia Reli ya Kati hapa nchini kususa-sua.

Kulingana na Wizara yenye Dhamana ya Uchukuzi, serikali ya Tanzania imeingia mikataba saba, ya Ujenzi wa Meli mbili mpya katika maziwa ya Victoria na Tanganyika,na ukarabati mkubwa wa meli nyingine tano.

Meli zitakazokarabatiwa ni pamoja na Mv. Victoria yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani  200 za mizigo.Meli hii ilijengwa mwaka 1960.

Nyingine itakayokarabatiwa ni  meli ya Kihistoria ya Mv. Liemba iliyojengwa mwaka 1903.

Meli hii yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo,hufanya safari zake kati ya Kigoma na Bandari ya Mpulungu nchini Zambia,katika ziwa Tanganyika.

Kuna Meli nyingine zinakarabatiwa, ili kujiweka tayari katika Soko la Afrika Mashariki(East African Common Market) na lile la Nchi za SADC.

Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulianza  tangu 1948 ukiwa na nchi tatu za Kenya,Uganda na Tanzania, Rwanda na Burundi kuongezeka miaka ya karibuni.

MV.LIEMBA KIVUTIO CHA UTALII

Ilijengwa mwaka  1903. Ina uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo. Husafiri kati ya Bandari ya Kigoma na Mpulungu nchini Zambia,katika ziwa Tanganyika,mara mbili kwa mwezi.

Hii ni meli kubwa ya Kihistoria,tangu zama za Msafara wa Watumwa kutoka hadi Congo kwenda Bara Asia na Ulaya kupitia Pwani ya Dar es Salaam.

Hii meli itakarabatiwa na Serikali, licha ya Kampuni hii ya Meli kusema itatengeneza meli nyingine mpya.

Meli hizi zitakuja kusaidia kusafirisha shehena ya mizigo ambayo sasa itakuwa na Bandari Kavu Misungwi, badala ya kutoka Dar es Salaam.

BANDARI YA FELA

Mamlaka ya Bandari(TPA), inajenga Bandari ya Nchi Kavu, Fela,wilayani Misungwi lengo likiwa kuvutia Nchi za Maziwa Makuu kupitisha shehena ya mizigo hapa Kanda ya Ziwa.

Bandari hii ya nchi kavu(Dry Port)katika eneo hili la Fela, inajengwa na Mamlaka ya Bandari Nchini(TPA),na ikikamilika inatarajiwa kukuza uchumi wa Mikoa yote ya Kanda ya ziwa.

Naibu Katibu Tawala Mkoa(RAS) hapa,Warioba Sanya,amesema Mradi huo unafuatia ziara ya Rais  Dkt.John Magufuli nchini Uganda mapema mwaka huu.

“Rais akiwa nchini Uganda,alifanya mazungumzo na Rais Yoweri Kaguta Museveni,wakakubaliana kushirikiana zaidi katika sekta ya Usafirishaji; miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni badala ya nchi hizo kufuata mizigo Bandari ya Dar es salaam,mizigo hiyo ichukuliwe Bandari Kavu ya Fela,wilayani Misungwi”,Naibu Katibu Tawala huyo amesema juzi.

Amefafanua kuwa Bandari ya Nchi Kavu ya Fela,itakapoanza kufanya kazi,itachochea kukua kwa uchumi wan chi na wananchi wa mkoa huu.

“Hata wenye nyumba za kulala wageni,mahoteli n.k watapata wateja wengi,kwa kuwa nchi hizi zitakuja hapa kuchukua shehena ya mizigo yao,badala ya kwenda Dar es Salaam”,Sanya amesema akiwataka wananchi kujiandaa kwa fursa mpya zinazokukaja.

Mamlaka ya Bandari(TPA) humiliki bandari za Mwanza Kaskazini na Kusini(Mwanza South na North Port),Nansio Ukerewe,Kemondo Bay na Musoma.

Vituo vingine vidogo vinavyomilikiwa na TPA ni Maisome,Nkome,Bukondo,Kahunda,Miharaba,Kome,Buchosa,Solima,Karumo,Chato na Nyamirembe(Kagera) na Kinesi mkoani Mara.

 Bandari ya Mwanza ni kiungo muhimu kwa nchi  zote za Maziwa  Makuu,hususan Uganda na Kenya,na huchangia kwa kiwango kikubwa kukua kwa shughuli za uchumi,hata katika nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki(EAC).

                         MIKATABA SABA

SERIKALI  kwa miezi ya karibuni ilikuwa ikitarajia  kutia saini jumla ya mikataba saba ya Ujenzi wa Meli mbili mpya za kisasa katika maziwa ya Tanganyika na Victoria, na kuzifanyia ukarabati mkubwa meli nyingine tano.

Kampuni ya Meli Nchini, Marine Services Company Limited, imesema Serikali sasa inatekeleza ahadi zilizotolewa na Marais wa Awamu Tatu za Utawala,tangu ilipozama Meli ya Mv.Bukoba,Mei 21 mwaka 1996.

Kaimu Meneja Masoko na Biashara wa Kampuni hii,MSCL,Philemon Bagambilana,amesema kati ya mwishoni mwa mwezi huu Juni au Julai,mikataba ya Ujenzi wa Meli Mpya za kisasa  Ziwa Victoria na Tanganyika,utasainiwa rasmi ili Meli hizo  zianze kujengwa katika Bandari ya Mwanza Kusini(Mwanza South Port) na Ziwa Tanganyika.

Meli mpya  ziwa Victoria,itajengwa na Kampuni kutoka Korea Kusini.

“Itakuwa na uwezo wa kubeba abiria,1,200 mizigo tani 400 za mizigo  na magari madogo 20…taratibu za manunuzi zimekamilika,mwishoni mwa Juni au Julai,mkataba huu utatiwa saini”,Bagambilana ameliambia Tanzanite jana.

Ahadi ya Ujenzi wa Meli Mpya ziwa Victoria ilitolewa kwanza na Rais Mstaafu,Benjamin William Mkapa,mara baada ya Mv. Bukoba kuzama mwaka 1996,ikaja kutolewa tena na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, kisha ikatolewa na Rais Dk. John Magufuli mara mbili akiwa ziarani katika mikoa ya Ukanda wa Ziwa.

Kufuatia hali hiyo,Meneja  Masoko na Biashara ameliambia Tanzanite kwamba,Kampuni ya MSCL iliyopewa Menejimenti Mpya na serikali ya Awamu ya Tano, inajenga Meli nyingine Mpya,ziwa Tanganyika.

“ Serikali inajenga meli nyingine mpya ziwa Tanganyika, itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo”,Bagambilana amesema huku akisisitiza Meli ya Kihistoria ya Mv.Liemba nayo kukarabatiwa.

“Meli ya Mv.Liemba inayosimama kama makumbusho ya Kihistoria tangu zama za misafara ya Watumwa, ambayo iko Ziwa Tanganyika,nayo inakarabatiwa, ina umri wa miaka 103, itafanyiwa ukarabati mkubwa ili iweze kuendelea kusafirisha abiria”, amesema Bagambilana.

Kampuni ya MSCL inamiliki jumla ya meli 14; tisa kati ya hizi zikiwa ziwa Victoria na tano zikiwa ziwa Tanganyika na Nyasa.

Kukamilika kwa meli mpya kumetajwa na wakazi wa Mwanza kuwa kutaondoa adha ya usafiri ziwa Victoria kwa kuwa kwa sasa meli zilizopo ni mbovu, na usafiri wa mabasi unatajwa kuwa aghali hususan kwa wasafiri wa miji ya Mwanza,Bukoba,Ukerewe na visiwa vya mikoa ya Geita na Kagera.

MV.SERENGETI

Ilijengwa mwaka 1988; ina uwezo wa kubeba abiria 593 na tani 350 za mizigo.

Husafiri kati ya Bandari ya Mwanza na Bukoba,Kemondo Bay mara tatu kwa juma.

MV.MWONGOZO

Ilijengwa mwaka 1982; uwezo wake ni kuchukua abiria 800 na tani 80 za mizigo. Meli hii haifanyi kazi sasa,imelala katika Bandari ya Kigoma ziwa Tanganyika.

MV.UMOJA

Iliundwa mwaka 1964,ni meli ya mizigo ambayo ina uwezo wa kubeba shehena tani 1,200  za mizigo au mabehewa 22 ya reli.

Meli hii ikifika Port Bell  na Jinja nchini Uganda, mabehewa hayo husafirishwa kwa reli kutoka Port Bell hadi mjini Kampala.

Zamani,ilisafirisha  pia mizigo kati ya Mwanza na Kisumu nchini Kenya au kati ya Kemondo Bay mkoani Kagera na mji wa Musoma kutegemea ‘Offer’ ambayo Kampuni ya MSCL iliyokuwa inapata.

Meli hii sasa imeanza kazi zake majuma machache yaliyopita, na serikali inasema itaikarabati ili iweze kuhimili kazi zitakazoletwa na Reli Mpya ya Standard Gauge,Bandari Mpya ya Fela na hata biashara itakayoanzishwa hapa Ushirikiano wa  Afrika Mashariki unapokwenda kuwa Shirikisho.

MT.NYANGUMI

(Motor Tug)Nyangumi ilijengwa mwaka 1958.

Ina uwezo wa kusafirisha tani 350,000  za mafuta. Hivi sasa iko Bandari ya Mwanza Kusini,ikisubiri matengenezo.

Hii ilisafirisha mafuta katika eneo hili kati ya Tanzania,Kenya na Uganda.

MV.SONGEA

Ilijengwa mwaka 1974; ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 43.5 za mizigo. Meli hii nzuri ilikuwa ikifanya kazi kati ya Bandari ya Itungi na Mbamba Bay.

Ilifanya safari zake mara mbili kwa mwezi huko ziwa Nyasa.Hivi sasa meli hii haifanyi kazi kwa sababu inasubiri matengenezo huko Bandari ya Kiwira.

MV.IRINGA

Iliundwa wakati mmoja na Mv.Songea mwaka 1974. Inabeba abiria 138 na tani tano za mizigo.Inasafiri kati ya BANDARI ya Itungi na Mbamba Bay(Malawi) mara mbili kwa mwezi.

Hivi sasa meli hii imelala Bandari ya Kiwia.

Ingekuwa inafanya kazi, bila shaka ingeinua uchumi wa wakazi wan chi hizi zinazopakana na ziwa Nyasa.

MV.BUTIAMA

Ilijengwa mwaka 1980.

Ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo kwenda na kutoka Nansio,Ukerewe umbali wa maili za majini 29 kila siku.

Hivi sasa imelala katika Bandari ya Kusini(Mwanza South Port),inasubiri ukarabati mkubwa,ambao mikataba inasainiwa majuma machache kuanzia sasa.

ML.WIMBI

(Motor Ligher)Wimbi,ilijengwa mwaka 1838 kwa lengo la kubeba tani hadi 120 za mizigo na kuisafirisha popote ziwa Victoria.

Ni meli ambayo ingesafirisha mizigo mahali popote kutegemea ‘Offer’ kampuni inayopewa ziwa Victoria. Mara nyingi ilisafiri kati ya Mwanza na Bukoba,Jinja(Uganda),Kisumu(Kenya) na mji wa Musoma.

Hii ni meli ambayo iliwasaidia wafayanyabiashara kwa kuingiza nchini au kusafirisha bidhaa na mazao ya wakulima kutafuta masoko katika nchi hizi.

MT(Motor Tug)Sangara

Iliundwa mwaka 1981 ikibeba jumla ya lita 410,000 za mafuta,ambazo ni sawa na tani 350. Hii iko Kigoma,Ziwa Tanganyika,ingeweza kusafirisha mafuta kutoka reline hadi nchi zote zinazopakana na Ziwa hili.

MT NYANGUMI nayo ni ‘Oil Tanker’ inasafirisha mafuta ziwa Victoria kati ya Mwanza,Bukoba,Jinja,Kisumu,Musoma na Port Bell.

MV. CLARIAS

Ilijengwa mwaka 1961 wakati nchi inajipatia uhuru kutoka wakoloni wa Kiingereza. Ina uwezo wa kusafirisha abiria 292 na tani 10 za mizigo kati ya Mwanza na Ukerewe kila siku.

Meli hii inafanya kazi baada ya Ukarabati.

MT.UKEREWE

Ilijengwa mwaka 1983 kazi yake ni kuvuta matishari.

Hizi ni meli nyingi kutosha kufanya mapinduzi ya kiuchumi hapa Maziwa Makuu,lakini eti Tanzania bado inalia umasikini wakati kuna fursa hizi tele,za kusafirisha biashara katika maeneo yote haya ya EAC,SADC n.k

Meli hizi zilikuwa zimekufa, zinafufuka wakati huu wa miaka mine ya JPM

 Afisa Mtendaji Mkuu huyu wa  Kampuni ya Meli nchini(MSCL) anasema:

“Nampongeza sana Rais Magufuli kwa jitihada za serikali yake kufufua miundombinu ya usafirishaji na mizigo katika Maziwa Makuu,hususan ziwa hili la Victoria. Hapa ziwa Victoria tuna meli saba; tatu zinafanya kazi”.

“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano,Dk. John Pombe Magufuli, kwa miaka yake minne ya Utawala ameleta mapinduzi makubwa sana hapa ziwa Victoria …ni mapinduzi makubwa yanayokuja hapa ziwa Victoria, kutakuja fursa tele za ajira na uchumi wakati wote wa ujenzi na ukarabati wa meli, sasa MSCL inageuka kampuni ya mkakati wa uchumi kimataifa”,amesema.

Kuna mapinduzi mengine makubwa ziwa Tanganyika.

Eric Hamissi anasema,

“utawala wa Awamu ya Tano, unalenga kufanya mapinduzi katika sekta za kimkakati kama hizi za usafirishaji wa abiria na mizigo hususan katika nchi zote za Maziwa Makuu za Kenya,Uganda,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,Rwanda,Burundi na hata Zambia na Sudan na Sudan Kusini.”

Eric Hamissi anaongeza kusema,

 “Mv. Clarias inafanya safari zake hata sasa kutoka Mwanza kwenda Nansio(Ukerewe) na kurudi jijini Mwanza kila siku.Mv.Clarias ina beba abiria 293.

Mv. Umoja husafirisha mabehewa kati ya Bandari ya Mwanza Kusini(Mwanza South) na mji wa Port Bell nchini Uganda.

Uwezo wa meli hii ya mizigo ni kubeba tani 1,200 za mabehewa. Sasa hivi tunamkataba na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi(WFP) tunasafirisha chakula cha wakimbizi kwenda Sudan Kusini kupitia Port Bell, na meli yetu hii ina reli ndani,inasafirisha mzigo huu hadi Kampala,Uganda kabla ya kusafirishwa kwa malori kwenda Sudan Kusini”,ana fafanua Afisa Mtendaji Mkuu huyu wa MSCL.

Kampuni hii ina meli nyingine,ML(marine lighter)Wimbi ambayo hukodishwa na wafanyabiashara kupeleka mizigo popote katika nchi zinazopakana na ziwa Victoria.

Mv.Wimbi ina uwezo wa kubeba tani 120  za mizigo.

MIKATABA YA UJENZI WA MELI MPYA

Septemmba 3,mwaka jana 2018,Rais Magufuli akiwa jijini Mwanza, alishuhudia utiwaji saini mkutaba wa Ujenzi wa meli mpya ziwa Victoria.

Meli hii ikikamilika baada ya miaka miwili itakuwa ikifanya safari zake kati ya Mwanza na Bukoba; uwezo wake utakuwa kuchukua abiria 1,200 na tani 400 za mizigo na magari madogo 20.

“Design’ inafanywa huko Korea, na meli hii  ikikamilika itasafirisha abiria hadi Kisumu nchini Kenya”,anasema Hamissi.

Meli hii mpya itaigharimu serikali jumla ya shilingi  bilioni 139 ambazo ni sawa na Dola za Marekani milioni 88.9.

“Sasa, tunatayarisha malipo ya awali ili meli hiyo ianze kujengwa hapa Tanzania na kukamilishwa katika kipindi cha miaka miwili”, Hamissi alifafanua mwaka jana 2018.

Anasema pia kwamba, wakati wa ujenzi wa meli hii mpya,wananchi takriban 500 wa Ukanda wa ziwa watajipatia ajira katika kipindi chote cha miaka miwili ya ujenzi wa meli hii kubwa ya kisasa.

UKARABATI  WA MWAKA MMOJA

Serikali ya Awamu ya Tano pia itatumia jumla ya shilingi bilioni 22 kuzifanyia ukarabati mkubwa meli kongwe za Mv.Victoria,Butiama na Serengeti.

Mv. Victoria iliharibika mwaka 2004.

Lakini, chini mkataba huu, meli hii itafanyiwa ukarabati mkubwa kabisa,itawekewa injini mpya na vifaa vingine vipya.

Butiama kabla ya kuharibika mwaka 2010 ilikuwa ikifanya kazi zake kati ya Mwanza na Nansio.

Mv.Serengeti nayo itafanyiwa ukarabati, mikataba inafanywa hadi sasa.

Uchumi umelala katika sekta ya usafiri. Kwa mfano ziwa Victoria Tanzania inapakana na Uganda na Kenya.

Uganda haina Bandari,huitegemea Tanzania kusafirisha bidhaa zake kwenda na kutoka ng’ambo.

Ujenzi wa meli mpya ya kisasa unaofanywa na Kampuni ya Korea Kusini  kwa kipindi cha miaka miwili Jijini Mwanza, unatazamiwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuajiri zaidi ya vijana 500  Ukanda huu hapa.

Meli hii mpya ambayo Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli alishuhudia utiaji saini  wake,Septemba 3 mwaka huu jijini Mwanza ,itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na tani 400 za mizigo; na ikikamilika itafanya safari zake kati ya Mwanza,Bukoba,Kemondo Bay,Port Bell nchini Uganda na Kisumu Jamhuri ya Kenya.

Afisa Mtendaji Mkuu(CEO)wa Kampuni ya Meli nchini(Marine Services Limited),Eric Hamissi, anasema, wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani wakae mkao wa kula, ajira 500 zinaletwa kwakati wa Ujenzi wa meli mpya ya kisasa, na ukarabati mkubwa wa meli zingine mbili, Mv.Victoria  na Mv.Butiama,zitakazowekewa vifaa vipya kabisa.

Huyu ndiye Rais Magufuli ambaye kila nikisikiliza redio za Wazungu wa Magharibi,zinasema ameharibu uchumi wan chi,anakandamiza demokrasia,nadhani tukikiri usemi kwamba, ‘Mnyonge Mnyongeni Haki yake Mpeni’.

Author: bundafm