MASANGOMA HATARINI KUBURUTWA KORTINI

WAGANGA wa  tiba asilia wako hatarini kufikishwa kortini kufuatia kuwauzia wateja wao dawa ambazo ujazo wake ni pungufu.

Waganga hawa wa dawa asilia,maarufu ‘masangoma’ wanadaiwa kuuza dawa za tiba za magonjwa mbalimbali katika vifungashio visivyoandikwa kiasi cha dawa kilichomo.

Meneja wa Wakala wa Vipimo(WMA)Mkoani Simiyu,Augustine Maziku,amewaonya masangoma na wauzaji wa dawa asilia,kwamba watakapokutwa wakiuza dawa hizi zisizoandikwa ujazo wala uzito kwenye chupa ama vifungashio vingine, watakamatwa na kupandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya wizi na utapeli.

Maziku amesema juzi  katika Baraza la Biashara wilayani Busega kwamba, kumezuka wimbi kubwa la waganga wa tiba asilia na wafanyabiashara wanaouza dawa hizi bila kuzingatia sheria za vipimo,kitu kinachozua janga kubwa la utapeli katika tasnia ya tiba asili.

Masangoma hawa pia wanadaiwa kutangaza sana dawa hizo kwamba hutibu magonjwa anuwai kwa wakati mmoja,kitu ambacho ni kinyume cha maadili ya tiba ya binadamu na mifugo.

Wimbi hili la wauza dawa za asili,limeenea sehemu kubwa ya nchi, na watu hawa dawa zao wanazitangaza kwa vipaza sauti vilivuomo kwenye magari, kitu ambacho ni kinyume cha maadili ya tiba.

Hairuhusiwi mtu kujitangaza kwamba yeye dawa yake inatibu magonjwa 30 au 50,wakati ukweli ni kwamba dawa hizo hazina ithibati.

Author: bundafm