MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA BUNDA WALIA NJAA

Na Jessica Mwita,Kibara-Bunda

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya  ya Bunda mkoani Mara wameilalamikia serikali kwa kushindwa kuwalipa stahiki zao kwa  miezi mitatu mfululizo.

Wakizungumza kwenye Ukumbi wa Kanisa Katoliki huko Kibara, baadhi ya madiwani wamesema wanahitaji kulipwa stahiki hizo pamoja na pensheni kabla ya Baraza kuvunjwa.

“Hatujalipwa stahiki zetu, na sasa Bunge likivunjwa na sisi madiwani hatutakuwepo, sasa lini tutalipwa”, mmoja wa Madiwani hao amehoji wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani (Full Council) huko Mjini Kibara.

Akijibu malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Amosi Kusaja, amewatoa hofu madiwani na kusema  watalipwa stahiki zao  baada ya maelekezo kutolewa na serikali. Hata hivyo, Mkurugenzi  huyu amesema ataweka mikakati na Kamati ya Fedha kuhakikisha malipo hayo yanafanyika kwa muda muafaka kutokana na mwongozo atakaopewa na serikali.

Mabaraza ya Madiwani yatavunjwa rasmi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Bunge.

Author: bundafm