KATUNI NI SANAA TU, SIYO KASHFA

 Kulingana na Compton’s Britanica Publications Vol. 4, ukurasa 145a mpaka 145c, katuni zimekuwepo tangu katika karne ya 19.

 Aghalabu, huchorwa katika kurasa za Tahariri za magazeti kutoa mtazamo bayana kwa ufupi, kuhusu habari ama tukio au matukio, yawe ya kawaida, ya kitaifa au ya kimataifa.

Siku hizi teknolojia imekua sana, katuni hutokea hata katika mindao ya kijamii.

   Katika karne ya 19 katuni zilitumika katika magazeti ya Uingereza kupeleka ujumbe kwa njia ya kejeli (satire); zikiwa na ujumbe uliotiwa chumvi, ili kuchekesha.

 Katuni ni mchoro au michoro inayozungumza lugha ya utani (joke) ili kuchekesha hadhira.

 Huchorwa kuhusu shughuli katika maisha ya watu, tabia, siasa au matukio ya kihistoria n.k. Katuni yaweza kufanya jamii kuanza kumcheka mtu au watu waliochorwa; lakini ukweli hubakia palepale, kwamba katuni ni utani tu juu ya tukio, mavazi, mitindo, michezo n.k.

 Ni ujumbe wa kuchekesha hadhira tu;huchukua taswira kwa njia ya kisanii ili kupeleka habari.

Ni michoro iliyotiwa chumvi, yenye kuandamana na maelezo mafupi (caption); ili kuchekesha au kustarehesha watu kuhusu tukio lililotokea.

 Inakisiwa kuwa katuni zimekuwepo zamani sana tangu katika Mapiramidi ya Wamisri, mapango ya Wagiriki na Warumi wa kale; ambapo hata watu maarufu au watawala walifananishwa na wanyama.

   Marais wa Marekani, kama Abraham Lincoln, nao walichorwa.

Mchora katuni maarufu Marekani katika karne ya 19, Thomas Nast (1840-1902) alipokuwa akichora katuni kuhusu chama cha Republican, alichora Tembo; na alipotaka kupeleka ujumbe fulani unaokihusu chama pinzani cha Democratic, alichora Punda!

   Hii huonyesha kuwa, kufananisha taasisi fulani kama vyama vya siasa, au Bunge na wanyama, hakukuanza jana.

Hakuna kumbukumbu kama Democratic walipata kulalamika kwa kuitwa punda!

Maana tembo ni mfalme (mtawala), lakini punda ni mtumwa wa watu (mtumishi wa umma)!

     Kufananisha watu, taasisi au hata mataifa na wanyama, hakukuanza leo.

Rumi ya zamani katika biblia hufananishwa pia na mnyama. Ugiriki hufananishwa na chui kutokana na falsafa zao,Babeli ilifananishwa na simba, na hata sasa Uingereza alama yao ni simba, Kenya pia ni simba, Uganda ni korongo(The Cranes), na sisi Watanzania ni mnyama mwenye madaha, Twiga!

Kulingana na Compton’s Britannica Publications Vol 2 uk 661, sanaa ni shemu ya maisha ya kila siku, na ya kila mmoja wetu.

 Ni muhimu katika kila tunachoona, tunachosikia n.k

 Tunapotembea barabarani mitaani katika miji,vijiji au majiji, tunapita majengo mbalimbali, mabohari, makanisa. Mengine huvutia, mengine hapana-haya yamejengwa na wajenzi ambao ni wanataaluma wa sanaa ya kale sana, naam sanaa inayoonekana kwa macho.

  Sanaa nyingine inayoonekana kwa macho ni nguo, samani za nyumbani, shule, makanisa n.k

Sanaa nyingine ni pamoja na muziki tunaosikiliza au kuona kwenye televishini zetu na siku hizi kwenye mitandao ya jamii na katika simu zetu za mikononi.

Muziki ni sanaa halisi, kucheza ngoma, lugha, insha, mashairi, tamthilia, michezo ya ucheshi(comedy), fasihi  ni sanaa pia.

  Kuna aina mbili za wasanii: Watunzi(Creators) ambao hutunga au kuandika kwa mfano wimbo ili uimbwe na waimbaji mahiri wenye talanta/vipaji.

Mtunzi(Dramatis) pia hutunga  tamthilia ili ichezwe na kuoneshwa jukwaani na kundi la waigizaji(actors).

 Mwalimu anayefundisha wachezaji kucheza ngoma ama dansi(a Choreographer) anapanga jinsi gani kundi lake litacheza .

Katika sanaa, waigizaji ni watu muhimu sana wanaotegemewa kufanikisha kazi za sanaa.

Tofauti na mpaka rangi, ambaye huwasiliana moja kwa moja na mtazamaji, sanaa nyingine kama ngoma,tamthilia ama ucheshi husubiri waigizaji ama wachezaji.

Hutegemea ufanisi toka kwa waigizaji.

Mtunzi Bingwa anapokuwa na waigizaji wabovu, kazi yake hushindwa kuonekana machoni pa wengi.

Msikose kufuatilia matangazo yetu mubashara kupitia, www.bundafm.co.tz

Author: bundafm