ACHENI KUPIGA WATUHUMIWA -POLISIWAONYA

Jeshi la Polisi wilayani Bunda,limewaonya wananchi kuacha mtindo wa kujichukulia sheria mkononi pindi wanapowakamata wahalifu.

Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilayani Bunda,Daudi Mathew Ibrahim amesema, ili kulinda amani na hakizi za msingi za Binadamu, watuhumiwa wote wanapaswa kukamatwa kisha kufunguliwa mashitaka mahakamani, kama watuhumiwa hao hawatakuwa katika mazingira hatarishi kwa taifa na kwa jamii.

“Raia wanapaswa kuacha kuwapiga na kuwaua watuhumiwa, kufanya hivyo ni kuondoa haki za msingi za watuhumiwa,wakamatwe na kufikishwa polisi au mahakamani”,anafafanua.

Akizungumza na Bunda FM,Bwana Daudi Ibrahim amesema kila raia wa Tanzania anapaswa kutekeleza wajibu wa Ulinzi shirikishi ili kuleta amani katika jamii.

“Suala la ulinzi siyo la polisi peke yao,bali raia wanapaswa kushirikiana na polisi ili kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani ili wajitetee,maana Mahakama ndiyo chombo pekee cha kutoa haki katika nchi, na mtuhumiwa huhesabiwa kwamba hana hatia hadi mahakama inapotoa hukumu vinginevyo”,amesema Mkuu huyu wa Upelelezi(OC CID)Bunda.

Ameongeza kusema kwamba askari waliopo katika jeshi la polisi ni wachache, wasioweza kutosheleza mahitaji ya ulizi wa raia na mali zao, kwa hiyo raia wana wajibu kushirikiana na Jeshi hilo la polisi katika kukabiliana na wimbi la uhalifu.

Hata hivyo,uchunguzi wa Bunda FM umebaini kuwa tabia ya wananchi wanaodaiwa wenye hasira kali kujichukulia sheria mkononi(mob Justice),hufuatia madai kuwa vyombo vya kutoa haki,vikiwemo polisi na mahakama huwaachia huru watuhumiwa bila kuwapa adhabu stahiki.

Madai haya yaliwahi kukanushwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu hapa nchini,Eliezer Feleshi, akiwa hapa Bunda alisema, Jamii imekuwa ikishindwa kutoa ushahidi mahakamani ili watuhumiwa wapewe adhabu.

“Watu wengi wanapowafikisha watuhumiwa polisi,huwa hawazingati kupeleka ushahidi mahakamani ili kuthibitisha makosa yaliyotendwa, badala yake watuhumiwa wanapoachwa huru kwa kukosekana ushahidi,hulalamika kwamba mahakama hazitendi haki”, Jaji Feleshi amesema hivi karibuni mjini Bunda wakati akikagua miradi ya taasisi hiyo nyeti.

Author: bundafm